Friday, January 15, 2016

BADO LIPO TUMAINI #2021 INAWEZEKANA.


BADO LIPO TUMAINI

#2021INAWEZEKANA.

2021 MWAKA WA KUFANIKIWA KWA CHOCHOTE MTU ATAKACHOANZISHA.

Mwaka wa kupanda na Kuvuna

Huu ni mwaka wa mtu ambaye hajakata tamaa ya kuanzisha jambo jipya au kuendeleza anachofanya.
Makanisa yanayokwenda kufanya Injili Bwana anakwenda kuleta mavuna mengi zaidi.

Mtu anatakayeinuka na kufanya tena atavuna mavuno mengi

Mhubiri 3:1
Kwa kila jambo kuna majira yake
Na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu.

Mara nyingi huwa tunajiuliza kwanini tunafanya mambo kwa juhudi na akili zote huku tukimtegemea Mungu lakini hatuoni matokeo makubwa.

Leo Roho Mtakatifu atufundishe kwa habari ya mpanzi.

Mathayo 13:3-9
3. Akawaambia mambo mengi kwa mifano, akisema, Tazama, mpanzi alitoka kwenda kupanda.
4. Hata alipokuwa akipanda, mbegu nyingine zilianguka karibu na njia, ndege wakaja wakazila;
5. nyingine zikaanguka penye miamba, pasipokuwa na udongo mwingi; mara zikaota, kwa udongo kukosa kina;
6. na jua lilipozuka ziliungua; na kwa kuwa hazina mizizi zikanyauka.
7. Nyingine zikaanguka penye miiba; ile miiba ikamea, ikazisonga;
8. nyingine zikaanguka penye udongo mzuri, zikazaa, moja mia, moja sitini, moja thelathini.
9. Mwenye masikio na asikie.

Hii ni ajabu,
Mpanzi alipopanda mara ya kwanza kwa bahati mbaya zikaanguka penye miiba, si kwamba aliangusha penye miba: hapana Yesu anasema zilianguka, kwa maana nzuri mpanzi alikusudia zianguke penye udongo mzuri lakini zikaanguka penye miiba zenyewe.

Ndiyo nimepanga sikukurupuka kufanya mambo lakini hayajafanikiwa. Yeshua anasema mwizi akaja akaiba.

Mkulima hakukata tamaa, si kwamba hakuumia, Yesu hakutaka stori iwe ndefu, ila mkulima aliumia tena sana. Lakini mwaka 2021 tujifunze toka kwake, hakukata tamaa, akainuka na kupanda tena.

Alipopanda tena Yesu anasema zikaanguka penye miamba, mbegu hizi pia si kwamba aliziangusha makusudi, hapana, alipanga mipango, alitumia akili na utaaramu wote lakini ni kawaida unapotupa mbegu zingine zinaanguka tofauti na matarajio.

Mbegu hizi zikampa matumaini mkulima, Yesu anasema zikaota, zikamfariji mkulima, tofauti na zile za mwanzo, lakini zikakosa mizizi hazikudumu zikafa.

Mkulima aliumia sana, kama wewe unavyoumia unapoona kuna vitu vinaanza kufanikiwa lakini vinakwamia njiani.

Tujifunze kwa mkulima 2021 hii, mkulima hakukata tamaa, akainuka na kupanda tena, alipopanda safari hii kukawa na afadhari, akapanda, safari zikaanguka penye miiba, Yesu anasema Math 13:22
Naye aliyepandwa penye miiba, huyo ndiye alisikiaye lile neno; na shughuli za dunia, na udanganyifu wa mali hulisonga lile neno; likawa halizai.

Yesu hasemi mbegu zilikufa, lakini anasema halizai. Mbegu imekuwa lakini miiba inausonga mti hata usizae.

Ni mengi tunayo tunayafanya katika mwili na katika ufalme wa Mungu. Si kwamba yamekufa ila yapo na hatuoni yakizaa.
Kuna mengi tunayo kama ni kazi, huduma au biashara. Yapo tu lakini hayazai. Hayatoi faida tunayoitarajia.

2021 tujifunze kwa mkulima, yeye hakukata tamaa, alitambua siri moja, kila jambo kuna majira yake, na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu.

Tuelewe jambo moja watu wa Mungu.
Majira ndiyo husema tufanye nini, na siyo tufanye nini husababisha majira fulani kutokea.

Mfano: kupanda mahindi hakuleti mvua, ila mvua husababisha tupande mahindi. Hivyo ili mahindi yaote ni lazima tusubiri mvua.

Vivyo hivyo, majira yanabadirika kila wakati yakizunguka ndani ya mwaka. Na kila majira yanatueleza nini cha kufanya.

Kipindi cha kiangazi ni kibaya sana, ni kipindi cha majaribu kila mbegu huangukia penye miiba, si kipindi cha kukaa ni kipindi cha kupita tu. Ila ni lazima mtu kupita ili ajifunze utii na kumjua Mungu.

Kipindi cha vuli hiki ni kibaya zaidi, majani yanapukutika, kila kitu kinaondoka, marafiki, tumaini, wakati mwingine hata amani na kibari, kila kitu kinaondoka. Musa amewahi pita huku, Yesu amewahi pita huku, hata wanafunzi wake walimkimbia, Paulo aliwahi pita huku, hata Watu wa Yerusalemu wakasema anafundisha Injili tofauti na ya Kristo, akaomba mara tatu udhaifu umtoke ikashindikana.
Hiki si kipindi cha kukaa, ni cha kupita tu.

Mkulima alijua haya, adui atakuja atachukua tu mbegu, maana ni majira ya vuli.

Masika, hiki ni kipindi cha neema, huleta tumaini jipya, imani na upendo mpya, kila mtu hutamani kukaa hapa. Kila upandacho kinaota. Na hii na ndiyo 2021.

Mkulima akaenda shambani akapanda, Yesu anasema ikazaa moja 100, zingine 60 na zingine 30. Hii ni njema sana Haleluya.

Mwaka huu ni wa kuanzisha vilivyoshindikana huko nyuma, ni mwaka wa kupanda upya tena. Kama ni biashara panda (anzisha), hata kama ilisimama, ilikufa, haizai, anzisha tena, kama huduma ilisimama anza tena, kama ni mikutano fanya ya kutosha. Kama ni kuowa na kuolewa anza mchakato tena, maana ni mwaka wa Bwana kuotesha vyote vilivyopandwa. Na havitachelewa.

MUHIMU
Huu ni wakati wa kumtumainia Bwana kuutafuta ufalme wake kuliko miaka yote. Kwa maana baraka nyingi zitawakuta hao.

Zaburi 37:5, Math 6:33, Isaya 40:31

Yesu hapendezwi na wenye hofu na mashaka, anapendezwa na wenye moyo wa imani, wanaokesha usiku na mchana wakitafuta ufalme wake na haki yake.

Yesu anasema mfano wa ndege wa angani ambao hawavuni, wala hawapandi, wala hawana ghara lakini Baba wa mbinguni huwalisha, je ninyi si zaidi ya hao.

Fikirini maua ya mashamba, jinsi yameavyo, hayafanyi kazi, wala hayasokoti, Yesu akaendelea kusema hata Sulemani na fahari yake yote hakuvikwa vizuri kama moja wapo ya hayo, Yesu akamalizia kusema Ikiwa Mungu huyavika hivi majani ya kondeni, yaliyopo leo na kesho hutupwa karibuni, je hatazidi sana kuwavika ninyi, enyi wenye imani haba. Mathayo 6:26-33

Kuna mambo ya kujifunza hapo, Yesu anasema "tafuteni kwanza ufalme wake na haki yake, na hayo yote mtazidishiwa"

Unapoenda kununua maharage, nyongeza ambayo unazidishiwa huwa hatuilipii, hapo tunakubaliana.

 Kitu cha kuzidishiwa huwa hakiitaji nguvu wala malipo. Unapewa bure.

Ila kuzidishiwa, ina maana kwamba kuna kitu ulikuwa umekifanyia kazi au umekigharamia. Na sasa mpaji anapokuja, anakupa ulichogharamia na ndipo kinafata kitu kinaitwa kuzidishiwa.

Ila kwanza umenunua, umetafuta, umepata cha kupewa kwanza.

Ila kama huna unachostahili kupokea (hujanunua kitu) , maana yake cha kuzidishiwa hapo hamna tena.

Hivyo ili ustahili kupata cha kuzidishiwa kwanza inatakiwa upate kitu kwanza (yaani utafute kitu fulani kwanza).
Ambacho ni kipi? Ni ufalme wa Mbinguni. Tafuta, toa gharama, kwa nguvu mpaka uuteke ufalme wa Mungu. Sasa ukishaiteka huo, ndipo muuzaji (mpaji) anakuja 2021 kuja kukuzidishia.

Mwaka 2021 hakikisha unang'ang'ania ufalme wa mbinguni kwa nguvu mpaka unauteka, na kama umeshauteka basi shikiria usiuchie mpaka upate ahadi zako ambazo ni kuzidishiwa, kufanikiwa katika kila jambo unalokwenda kulifanya.

Sasa, elewa mfano wa ndege, Yesu hapendi watu wenye hofu na waliokata tamaa ya kupanda. Tazama ndege anapoamka asubuhi, anakuwa ana imani kuwa Baba wa mbinguni ameandaa pumba sehemu nitaenda kula.

Wewe anzisha biashara, anzisha mradi, anza huduma, anza mpango wa ndoa, anza chochote, kisha wateja, washirika, mchumba, au support hilo wewe amini tu, nyanyuka Bwana ameshaandaa. Hiyo siyo kazi yako.
ANGALIZO: ndege hakuwahi tengeneza pumba. Wengi wanaziba nafasi ya Mungu kwa kutumia mpaka njia zisizo harali kulazimisha kutengeneza pumba, acha nafasi ya Mungu.

Mfano wa maua: Maua hayana shida, yenyewe yanafanya kazi moja tu, hayaondoki kwenye udongo: usiondoke kwa Mungu. Kisha yanatoa mizizi yake, yakiamini Mungu ameandaa maji sehemu nitakwenda kuyanyonya.

Ebu fikiri Sulemani pamoja na utajiri wake wote, aliweza kupata chochote alichokitaka, chochote ambacho moyo wake ulikitamani, lakini bado Yesu anasema maua yamevikwa zaidi ya Sulemani, lazima Yesu kuna kitu anajua sisi hatujui.

Lakini nini maua yanafanya, moja hayatoki kwenye udongo: usitoke kwa Mungu tafadhari, mbili yanatoa mizizi.

2021 ni mwaka ambao Bwana amendaa masika ya ajabu sana, toa mizizi yako.

Anzisha biashara tena, panda tena. Fanya chochote, anza kilimo au mifugo,chochote, na Bwana anakwenda kutoa maji.

ANGALIZO: Maua huwa hayapeleki mizizi mahari pasipo na maji.

Muombe sana Mungu akuongoze wapi upeleke mizizi.

Usiwe mkuyu, unaolazimisha kupata maji wakati wa kiangazi na kulazimika kuwa na mizizi mirefu sana, ili kupata maji yalipo.

Kufanikiwa kwa njia ndefu sana kunachosha sana, omba Mungu masika ije, ujue maji yalipo, haraka uchomoe mizizi na uanze kuvuna zabibu Katika Jina la Yesu.

Kumbuka kujifunza kwa mpanzi, kwa ndege wa angani na kwa ua.

Kwa msaada wa Roho Mtakatifu somo hili limeandikwa na Kuhubiriwa Tarehe 31/12/2020 saa 4:42 - 5:26 Usiku.
Na
Pastor Ulenje EM.
Na kutumwa kama somo maalumu kwako. 


NA IKAWE KWAKO KATIKA MEMA SOMO HILI KWA JINA LA YESU. 

0683 477827
0718 721848


No comments:

Post a Comment