Wednesday, March 16, 2016

Part 6: MAANDALIZI MUHIMU KABLA YA KUSEMA NDIYO....

MAANDALIZI MUHIMU KABLA YA KUSEMA NDIYO...

Mithari 16:1
"Maandalio ya moyo ni ya mwanadamu;
Bali jawabu la ulimi hutoka kwa Bwana.

Tumetoka mbali na leo tufike tamati, jitie nguvu kusoma maandalizi yote ni ya muhimu. Nakusihi usikose hata Part moja ya somo hili, bonyeza sehemu iliyoandikwa "home" na uanze na hili somo kuanzia Part 1 mpka 6. Hapo utakuwa umefanikiwa kupata semina hii yote. Tulioanza pamoja Mungu awabariki sana. Semina ijayo ni muhimu sana "TABIA NA UTUMISHI" usikose.
Tuendelee...

7. Je Upo Tayari Kumfanya Mwingine Awe na Furaha na Amani .

Karibu kila binaadamu amezaliwa na ubepari ndani yake, yaani ubinafsi. Popote hutazama anapata nini, hata yule atendae kwa wengine basi huwa na fikira kuwa Mungu atamlipa au kumbariki. Huwezi kufanya jambo pasipo kujitazama wewe.

Jambo ambalo mwanadamu yeyote analitafuta ni amani na furaha. Anataka chakula ili awe na furaha, anatafuta pesa ili awe na furaha. Nimewahi ona watu wenye pesa pasipo kuwa na amani kwenye ndoa yao, na watu masikini wenye amani na furaha kwenye ndoa yao.

Usisahau, jambo gumu kulitafuta kuliko yote hapa duniani ni amani. Ndiyo maana Biblia imesema "tafuteni..." Maana yake amani ni ya kuitafuta.

Ni vema ukajifunza nini huwafanya wanawake wawe na furaha na nini huwafanya wanaume wawe na furaha kabla ya kuingia kwenye ndoa. Ni vema ukajifunza kutafuta amani hata wakati ambapo umekosewa na kuchukizwa.

Mtu mmoja aliwa kunishangaa, baada ya kuona ananieleza jambo la kutisha ambalo watu wamenifanyia, lakini mimi nacheka. Alitegemea nitahuzunika na kuchukizwa sana. Kwanini Mungu amenisaidia kujua maana ya amani na kuitafuta hasa pale ambapo haipo au inataka kutoweka.

8. Je Unajua Kusamehe

Kwa haraka waweza kujibu "ndiyo" lakini fikiri wangapi si marafiki zako tena kwasababu tu umeshindwa kuwasamehe, au umesamehe makosa tu! Bado hujawasamehe wao, na ndiyo maana si marafiki zako kwa sasa.

Nisiwe na maneno mengi hapa, ila niseme tu, palipokuwa na wawili basi ndipo makosa huonekana, na kila mtu hujiona bora pale aonapo makosa ya mwenzie. Na kama watu wengi bado hawajakamilika, bado wana hisia zinazowashinda kuzikabiri kama hasira, chuki, wivu na mengine, kama kila mtu huwa anakosea. Ipo haja ya kuamini hata huyo unayesema ndiyo kwake basi ipo siku atakosea.

Basi nina uhakika upo umuhimu mkubwa wa kujifunza kusamehe hata makosa yasiyosameheka, hata pale mwenzio anaona hana haja ya kuomba msamaha. Naamini itakusaidia, lakini kama hujui kusamehe, kila kosa unataka useme, kila wakati unataka uonekane uko vema na mwengine amekosea basi vema ukaomba pooooo....kabla hujaanza uhusiano na mwenzio.

Unajua maana ya kutokusamehe ni kujisemea moyoni mwako hivi "yaani huyu mtu asiyekamilika, mdhambi ananitendea unyama mimi niliyekamilika, mtakatifu na nisiyekosea hata mara moja!!!!...." Hayo ndiyo maneno uyasemayo pindi unapokataa kusamehe. Jifunze kusema "nimekusamehe hata kama hujaombwa msamaha....ndipo useme ndiyo.

9. Je Una Tabia ya Ndoa

Naamini watu wengi hutazama umri wao na si tabia zao, na ndiyo maana wengi wameolewa na kuowa wakiwa bado.

Umri huletwa na miaka, tabia huletwa na mafunzo na fikra. Umri tunatazama miaka, tabia tunatazama matendo na fikra.

Nimeona ndoa za wengi walioowana wakiwa wadogo sana mpaka leo wanadumu na kuendelea nikiwatembelea huwa naona vicheko si vya uongo bali vya kweli. Na nimeona wapo walioowana wakiwa na umri mkubwa na ndoa zao hazijakaa salama hata vicheko vyao ni vya kudanganya wageni.

Siku ya leo maarifa yameongezeka, hatuna tena tatizo la maarifa bali tuna tatizo tu la kuwa na maarifa mengi. Nafikiri ni vema ukachambua na kutafuta maarifa ya KiMungu, wapo watumishi wengi waliofanikiwa kwenye ndoa Zao na wamejitahidi kuandika na kufundisha maarifa mengi ya ndoa. Kuwa msomaji, badiri ratiba ya matumizi ya smartphone yako, anza kusikiliza mafundisho ya Mungu, soma blog zao, soma vitabu vyao. Ili upate kujua maarifa hayo.

Maandalio ya moyo ni ya kwako, ila jawabu ni la Bwana. Usitazame umri na miamko ya mwili: tazama je una tabia za ndoa, je unaweza kuishi na mti mwingine na kuendana na tabia, udhaifu na utofauti wake. Usije ukawa unamsubiri Mungu, kumbe ni Mungu ambaye anakusubiri wewe.

Kila kitu kina tabia yake, na usipoifata hutofanikiwa. Kuna tabia za biashara, kuna tabia za kilimo, kuna tabia za wanasiasa, kuna tabia za wanafunzi, kuna tabia za wachungaji. Vivyo hivyo na ndoa, kuna tabia ndoa inahitaji uwe nazo.

Mfano; unajua kujari, unajua kusamehe, unajua kuchukuliana na watu, unajua thamani za watu pachoni pako, unajua kujitoa kwaajili ya mwingine, unajua kupika, unajua kusaidia, unajua kujitoa hata kama umechoka, unajua kuonesha utii hata kwa aliyekuudhi.

10. Je Umejiandaa kwa Matokea

Ndiyo yako ya kuingia kwenye ndoa ina matokeo na baada ya kusema ndiyo vitu vingi vinatarajiwa kutokea. Kwa haraka, tunatarajia watoto, kupungua kwa baadhi ya maamuzi yako binafsi, kupungua kwa uhuru wako, kuingiliwa maamuzi na mwingine, kuongozwa na mtu mwingine, kuongezeka kwa majukumu.

Ni vema ukajiandaa na matokeo hayo hata kabla ya kusema ndiyo. Haina maana ya kufikiri kuyakabiri yote kwa wakati mmoja bali ni kujiandaa nayo.

11. Je umejiandaa kukabiri Mabadiriko ya mtu.

Binaadamu siyo jiwe kwamba habadiriki.

Watu wanabadirika kiuchumi kushuka au kupanda, wanabadirika muonekano wa mwili na uzuri wao, mabadiriko ya nguvu, fikra na baadhi ya tabia, wanabadirika matendo, hata imani kuna wakati wanashuka na wakati wanapanda kiimani.

Mabadiriko hayo yanapotokea: ni wakati wa kiangazi ambapo kila mtu anahitajika kuwa imara kuhakikisha boti haizami ndani ya maji.

Ni jambo linaweza kuoneka dogo, lakini kama usipoandaa ufahamu wako kujiandaa katika hili, kiangazi kijapo na kukukuta hauna chakura utakuwa kwenye shida.

12. Je una Uwezo na Upo tayari  Kujitoa

Upendo ni kujitoa, kwa hari na mari. Huwezi kusema unampenda mtu na haupo tayari kujitoa kwaajili yake, na kila mtu anatamani mtu anayejitoa kwaajili yake.

Kuna vitu huwezi kufanya pasipo kujitoa. Jiandae. Kuna wakati wa kuchukizwa: ni kujitoa kusamehe. Kuna wakati wa kuchoka na kutokuwa na kitu kabisa, kuna wakati wa kusaidia hata kama huna uwezo.

Kujitoa si kitu kidogo kinahitaji upendo wa dhati sana (deepest love) na kama huna upendo huu hutoweza.

Nina mengi ya kusema ila Roho Mtakatifu ndani yako atakufundisha mengi zaidi.

Kipimo kikubwa cha somo hili: Kumbuka nini kilikuachanisha na rafiki zako au wapenzi wako wa zamani, pia tazama ni nini ambacho hukipendi na kinakuchukiza kwa mke au mume wako, au mchumba wako. Utagundua uliacha nao urafiki au uchumba ni moja ya maandalizi haya hukuwa nayo, na hata sasa huridhiki kwasababu moja ya maandalizi huna.

Kuna KITABU kipo jikoni "BADO LIPO TUMAINI" utakapokiona dukani tafadhari nunua. Na zidi kuomba kwa habari ya watumishi.

Natamani kupata comment yako, phone call au whatsapp.
+255 718 721848
imaf2b@gmail.com

Monday, March 7, 2016

Part 5: MAANDARIZI MUHIMU KABLA YA KUSEMA NDIYO...

MAANDARIZI MUHIMU KABLA YA KUSEMA NDIYO...

Bado Tunazidi kuchana Nyavu...
#SeminaKiganjaniMwako.

4.  Je upo Tayari Kubadirishwa, Kukosolewa, na Kuboreshwa

Moja ya hadithi niliyowahi kuisoma darasa la kwanza na  nisiyoisahau ni hadithi ya "Mti wa Mpapai uliogoma kwenda huku-na-huku kuufata upepo" upepo ulipozidi, mpapai ukaanguka.
Tunafahamu kuwa kila binaadamu ana udhaifu, ila Mungu ametupa uwezo wa kuwa wakamilifu: na hutumia watu wa karibu, matukio na majaribu katika maisha.
Naamini tunaingia kwenye ndoa si kushindana bali kukamilishana: ili kutimiza kusudi ambalo Mungu ameliweka katika maisha yetu.
1 Kor 11:11 "Walakini si mwanamke pasipo mwanamume, wala mwanamume pasipo mwanamke, katika Bwana"

Nikupe siri; Udhaifu wa mtu hugunduliwa na mtu mwingine hasa wa karibu yake sana" Dr Myles Munroe aliwahi toa mfano kusema "Ni vigumu kujua kuwa kiatu chako kinatoa harufu mpaka mtu mwingine akwambiye"

#Kama wote tupo kwenye safari ya kuelekea ukamilifu, na tunahitajiana ili kuwa wakamilifu, na tunafurahiana hasa pale tunapoonesha ukamilifu: basi kuwa tayari kuelimishwa, kupokea mafundisho mapya, fikra mpya, mipango mipya, na kuboreshwa baadhi ya tabia zako, ni MAANDARIZI YA MUHIMU SANA"

5. Je upo Tayari Kuacha Baadhi ya Vitu Unavyovithamini Kwaajili ya Mahusiano.

Idadi kubwa ya wachumba wameachana kutokana na kupishana na misimamo na mitazamo ambayo kila mmoja anathamini. Hata wanandoa wengi; mabishano yao makubwa mara nyingi, ni pale misimamo, mitazamo na fikra zinapogongana.
Misimamo; ni falsafa na mawazo ambayo mtu huamini kuwa ni sawa na yanapaswa kufatwa na wote ili kupata mafanikio.
#Kama hampo tayari kukaa chini na kujiandaa kupanga misimamo, mitazamo na falsafa ya pamoja na kuacha ya binafsi basi ni heri mkaomba pooooo! Kabla ya kusema ndiyo!! Na mkaendelea kukuza akiri zenu.

Maana mtakaposema ndiyo! Pasipo kuwa tayari kuacha baadhi ya misimamo ambayo inaweza kuwatenganisha, na kuunda misimamo ya pamoja; Itakuwa haina maana, sababu safari yenu itakuwa fupi.

6. Je Unaweza kulinda Maono yako; Huku Ukitimiza Kusudi la Pamoja.

Mwanzo 2:18;5:1
Hii ni mistari dhahiri inayoonesha kuwa Mungu ametuumba kutimiza kusudi moja pale tunapoungana na kuwa mtu mmoja; tofauti ni kwamba mmoja mjenzi, mwingine saidia.
Ila saidia asiyekuwa na maono, hafai, na mjenzi asiyekuwa na maono hafai kitu.
Saidia ni lazima maono yake yaendane na maono ya mjenzi, na kusaidia kusudi la pamoja kutimia.
Na mjenzi ni lazima maono yake yajulikane, yaendane na saidia wake; ili aweze kumsaidia.
Kusudi ni juu ya maono: Kusudi ni "Sababu ya wewe kuzaliwa" na maono ni "Kioo cha kutimiza kusudi lako na namna ya kufika kwenye kutimiza kusudi lako"

#Hivyo wote wawili muwe tayari kuunda maono yenu yaendane na safari ya kufika kwenye kusudi ambalo Mungu amewaumba kutimiza"
Haleluya!!!!

Sifa na Utukufu apewe Bwana
Kwa msaada wa Roho Mtakatifu tunazidi kuenderea