Friday, July 16, 2021

NAMNA YA KUWA MWANAFUNZI BORA WA YESU

25/06/2021, PREACHED 27/06/2021 AT VICTORY EMPOWERMENT TEMPLE 

FANYIKA MWANAFUNZI

WEWE NI ZAIDI YA JINSI ULIVYO. UNAWEZA KUWA ZAIDI YA JINSI ULIVYO LEO.


Yesu aliwakuta wanafunzi wake wakiwa wavuvi, hata Galilaya walikuwa hawafahamiki, lakini walipofanyika wanafunzi, wakafika mpaka kwa Wayunani, mpaka Asia. 
Unaweza kufanyika zaidi ya jinsi ulivyo leo, kwa sababu unaweza kufanyika mwanafunzi. Kufanyika mwanafunzi wa Yesu ni daraja la kukuvusha daraja la maisha, ni ngazi ya kupanda ngazi nyingine ya maisha. Kama unawaza wapi pa kuanzia ili upae kimaisha, basi anzia na kufanyika mwanafunzi wa Kristo.

Kusudi la Kristo ni Kujipatia Watumishi.

Math 28:19, Yesu anasema, “Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu;
Yesu anaweka wazi, anataka wanafunzi. Na ukweli hajatutuma kukufundisha bali kukufanya mwanafunzi. Yesu amekuokoa ili uwe mwanafunzi.
Yesu anasema “Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu; MATH 11:29.

Ukisoma mstari wa juu yake ‘28’ anasema “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha”. Kusumbuka iwe mwisho_ umekopa sana kufanikisha mipango, umeomba, umetafuta, umelia_ leo nenda kwa Yesu_ kanunue Biblia sema “nitajifunza kwa Mungu nami nipumzike, nipate raha”

Kwanini uwe mwanafunzi?

1. Sababu mwanafunzi pekee ndiye unaweza kumbadirisha. 
Anayekufundisha anakufanya uwe mtu fulani_ na hasa anakufanya yeye alivyo. 
Yesu hataki ujifunze kwa dunia, kwa sababu ukijifunza kwa dunia utakuwa kama dunia. Ila ukijifunza kwa Yesu utakuwa kama Yeye. Yesu anasema “Mwanafunzi hawi mkuu kuliko mwalimu wake, lakini kila mtu ambaye amehitimu hulingana na mwalimu wake”. LUKA 6:40. 
Yesu anataka uwe kama yeye. Na dunia wanataka uwe kama wao_ lakini wote hao ni wageni hapa duniani, Yesu ni zamani kuliko wote_ wote wameikuta Biblia_ na ina shuhuda ya kufanikisha wengi_ ni bora leo ukachagua kuwa mwanafunzi wa Yesu. 
Unapofungua Biblia na kusoma, unafanyika neno, unafanyika kama Yesu.

     ✅ Yesu Akawaambia, Nifuateni, nami nitawafanya kuwa wavuvi wa watu” MATH 4:19. Yesu anataka akubadirishe kutoka mtu fulani uwe mtu mwingine, 
Kila aliyeamua kufanyika mwanafunzi_ baada ya mda fulani, watu wakasema “siyo yule tunayemjua” wengine kwa mshangao wanasema “ni wewe kweli, au mwingine”
  Paulo anasema “Na wale aliowachagua tangu asili, hao akawaita; na wale aliowaita, hao akawahesabia haki; na wale aliowahesabia haki, hao akawatukuza. ROM 8:30. TENA Anasema “tunabadilishwa tufanane na mfano uo huo, toka utukufu hata utukufu, kama vile kwa utukufu utokao kwa Bwana, aliye Roho. 2 KOR 3:18.
Usijipime leo, Hayo unayopitia ni milima na mabonde tu ya njiani_ fanyika mwanafunzi_ wewe ni zaidi ya jinsi ulivyo. Kuna mtu Yesu anamtengeneza mwenye utukufu zaidi ya ulio nao leo. 

2. Sababu anataka akujulishe siri za ufalme.
Ukishasikia siri, maana yake kuna watu maalumu wanaostahili kujua. Yesu hakuja kumwambia kila mtu siri za ufalme wake, bali wanafunzi wake pekee. Yesu anawaambia wanafunzi wake “Ninyi mmejaliwa kuzijua siri za ufalme wa mbinguni, bali wao hawakujaliwa” MATH 13:11. 


3. Sababu anataka akutumie.
Yesu hajawahi kutumia mtu ambaye hajafanyika mwanafunzi. “watu wengi walimwamini…lakini Yesu hakujiaminisha kwao; kwa kuwa yeye aliwajua wote; YOH 2:23, 24. Kumwamini haina maana yeye amekuamini, na sifa ya kumuamini siyo kuwa mkamilifu, bali kuwa mwanafunzi. Pamoja na udhaifu alio nao Petro, lakini Yesu alimvumilia na akamuachia kanisa, kwanini_ wakati wengine wamekimbia, yeye akasema “Twende kwa nani? Wewe unayo maneno ya uzima wa milele, YOH 6:68.
Mungu sasa anataka kutumia watu wa kila sekta, wafanyakazi, wafanyabiashara, wakulima, waimbaji ili kujipatia mavuno na kutangaza jina lake_ ili kuipa aibu dunia… wewe fanyika mwanafunzi. Naye atakutumia. 

Siyo Kila Mtu ni Mwanafunzi.

Kwenye biblia kuna makutano na wanafunzi. Kuhudhuria kanisani na kuokoka haina maana wewe ni mwanafunzi.
Unaweza ukahudhuria kanisani miaka 40 lakini usiwe mwanafunzi, kwasababu uwanafunzi siyo miaka uliyookoka, wala uliyohudhuria kanisani, uanafunzi ni maamuzi, siyo kuhudhuria. Wote ni mashahidi hasa kwa walimu ambao wanachapa sana, tulikuwa tunahudhuria darasani lakini tunasikia lakini hatusikilizi. 
Yesu anasema “Kusikia mtasikia, wala hamtaelewa; Kutazama mtatazama, wala hamtaona. MATH 13:14, 15.
15. Maana mioyo ya watu hawa imekuwa mizito, Na kwa masikio yao hawasikii vema, Na macho yao wameyafumba; Wasije wakaona kwa macho yao, Wakasikia kwa masikio yao, Wakaelewa kwa mioyo yao, Wakaongoka, nikawaponya. 

Tunajuaje kuwa wewe ni mwanafunzi?

NAMNA YA KUWA MWANAFUNZI WA YESU.

Tuone sasa namna, unaweza kuwa mwanafunzi. Ni vigezo gani mwanafunzi anavyo.

1. Mwanafunzi Analiamini na Kulikubali Neno Lote.
Siyo nusu, siyo moja_ yote. 
Yesu siku zote alitumia maneno magumu ili kuchambua wanafunzi na makutano. Biblia inasema “wengi miongoni mwa wanafunzi wake wakarejea nyuma, wasiandamane naye tena” wakakimbia wote, wakabaki wanafunzi tu. YOH 6:64-69. 
 Nao akawauliza “Je! Ninyi nanyi mwataka kuondoka?” Petro akajibu akasema “Twende kwa nani? Wewe unayo maneno ya uzima wa milele, Nasi tumesadiki, tena tumejua wewe ndiwe Mtakatifu wa Mungu”. Mwanafunzi anaamini yote. Paulo anasema “…nikiyaamini yote…” MDO 24:14. 
Na huwezi sema umeamini mpaka umekubali ulichosikia, umekipokea na kukitendea kazi ulichosikia. 
Huwezi sema ni mwanafunzi mpaka umekubali, na kukishika kile mwalimu amesema. Na mwalimu wetu ni Yesu, na shule yake ni Biblia. Na anatumia watumishi wake kukueleza alichoandika. Paulo hajaandika Biblia, Mathayo hajaandika Biblia, mimi sijaandika Biblia_ wote waliandika yale Roho Mtakatifu amesema, nami nahubiri yale Biblia imesema. Nami natenda hayo hayo na naona matokeo, na Mungu amenituma nisema nawe, ili tuinuke pamoja.


2. Moyo wa unyenyekevu.
Pasipo moyo wa unyenyekevu huwezi kumfundisha mtu yeyote. 
Mtu mwenye kiburi anajua kila kitu, hata ambacho yeye mwenyewe anajua kuwa hajui. Lakini atalazimisha kwa maneno mengi kuwa anajua. 
Watu kama hao_ hawawezi kuwa wanafunzi. Sababu wanaenda kwa Mungu, huku wakiwa na ya kwao. 
Wanasema Mungu tufundishe, lakini kama ni kinyume na aliyosema mjomba, bwana vicoba, hatuwezi kukusikiliza.
Hakuna kazi ngumu kama kumfundisha mwanafunzi mwenye tution nyingi.
 
Yesu anasema “kwa maana kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa” LUKA 14:11. Unafikiri kwanini Mungu anainua wanyenyekevu, kwa sababu mnyenyekevu ni kama mtoto anabebeka (Math) anafundishika,
Mungu anasema “…Mimi ni BWANA, Mungu wako, nikufundishaye ili upate faida, nikuongozaye kwa njia ikupasayo kuifuata. ISAYA 48:17

Kiburi hutangulia uangamivu; Na roho yenye kutakabari hutangulia maanguko. MITH 16:18.

3. Mwanafunzi wa Yesu  Anakuwa.

Sifa ya mwanafunzi ni kukuwa. 
Kila mwalimu anapima mwanafunzi wake kwa kukuwa katika kile anamfundisha. 
Haijarishi umetokeo wapi kwenye wokovu, lakini kila siku inabidi ukue kila eneo_ kuomba, kusoma neno, kuhudhuria ibada, kufunga, kushuhudia.
Yesu anasema “Naye aliyepandwa penye udongo mzuri, huyo ndiye alisikiaye lile neno, na kuelewa nalo; yeye ndiye azaaye matunda, huyu mia, na huyu sitini, na huyu thelathini. MATH 13:23.

4. Mwanafunzi lazima awe ametubu.

Yesu anapoanza injili yake tu_ akasema nini ufanye ili uwe mwanafunzi wake.
Tokea wakati huo Yesu alianza kuhubiri, na kusema, Tubuni; kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia. MATH 4:17

Kutubu siyo kuomba msamaha, ni zaidi ya hapo. Kutubu ni kubadiri unavyowaza, kubadiri mfumo wa maisha.

Yesu anaweka wazi, nimewakuta mna ufalme wa dunia hii, sasa geukeni acheni kuwaza na kufanya kama dunia, sasa muwaze na kufanya mambo kama ufalme wa mbinguni unavyotaka.

Others
5. Usiogope watu
Huwezi kuwa mwanafunzi kama unaogopa watu wanasema nini. Sababu siku zote Yesu anakwambia mambo ambayo watu hawataki, ni kinyume na wanavyojua, ni kinyume na wanavyotaka uishi. Kilichomponza Sauli ni kuogopa watu, akaacha kufanya Mungu alichomfundisha.
Yesu akasema 
6. Jikane mwenyewe_ luka 14:26
7. Beba msalaba wako_ luka 14:27

Hitimisho.
Omba unyenyekevu na maombi ya agano_ kuwa wanafunzi. Na weka agano kutenda nini neno linasema.

Ushauri au maombi.
0683 477 827 
0718 721848 

Thursday, January 21, 2021

NAMNA HII HUPONYA NDOA MARA 100 ZAIDI.


Jambo hili likikosekana, mwanamke atachanganyikiwa, Mwanaume atakuwa wa lawama siku zote.

Nimetazama ndoa nyingi za mwanaume mvivu asiyejua majukumu yake.

Mwanamke akitazama kila kitu alichovaa ndani na nje, simu na vocha, na kila kitu alichonacho, kimetoka kwa mwanaume, Si tu, Atajivuna kwa marafiki, Lakini ATAKUHESHIMU na UTAMTAWARA.

MUNGU hakumpa Hawa Bustani, alimpa Adamu, Mungu hajawahi kumwambia Hawa ailime bustani, bali alimwambia Adamu, hata neno la kusema "matunda ya kila mti wa bustani waweza kula" MWA 2:16 hakumwambia Hawa, alimwambia Adamu.

Ina maana jukumu la kula na huduma, ni la Adamu kwenye familia, siyo Hawa. Ndiyo maana siku moja, siku moja tu, haikuhitaji nyingi, Adamu alipopumzika na kumuacha Hawa akajitafutie chakula, ndipo shetani anajitokeza, na ndipo anguko la familia ya kwanza linatokea, na madhara hadi sasa duniani tunayaona.

Nionyeshe familia ambayo, mwanamke anahusika kutafuta chakula, nitakuonyesha familia ambayo shetani amejenga nyumba karibu nao. Na ipo siku atawadondosha, as matter of time. GOD FORBID.

Hata uchumba ambao mwanamke ndiye chanzo cha pesa unahitaji mabadiliko.

Mwanaume asiyefanya kazi na kuhudumia mke wake na watoto, asitegemee kupata heshima na asiwe na tarajio la kumtawara mke wake. Biblia inasema...

Mithali 12 24
Mkono wa mwenye bidii utatawala; Bali mvivu atalipishwa kodi.

Ukiwa na bidii, bila hata kumwambia "niheshimu" bali akitazama wewe ndiyo chanzo cha kupendeza kwake, chanzo cha kula yake, chanzo cha kila kitu alichonacho. ATAKUHESHIMU automatic. Mwanamke anaheshimu sana chanzo cha heshima yake, shika sana hili neno.

Nikiwa nasoma chuo kikuu cha Dar es Salaam, nilikuwa nasoma huku nafanya biashara stendi ya Ubungo, asubuhi naamka naenda Kariakoo kufata bidhaa, ndipo naenda chuo. Jioni naenda kanisani kuonyesha sinema watu waokoke, nikirudi moja kwa moja maktaba kusoma, nilikuwa naomba mara nne hata zaidi kwa siku. Nilikuwa sina mkopo lakini kuna watu wenye mkopo niliwakopesha pesa.

Kwa neema ya Mungu sijawa pata Disco, Wala sijawa Carry, Wala sijawahi fanya SAP, Na bado msimu wa mvua nilirudi Morogoro kulima, maana nilikataa kula unga wa dukani kwenye maisha yangu, na mchumba wangu alitumia Smartphone ambayo mimi nilinunua na nilimuongezea pesa za kutosha katika biashara yake. Kwanini nilikataa kuwa mvivu.

Nakumbuka watu waliniita speed man, sababu nilikuwa natembea speed ni hatari.

Vijana wa kizazi hiki Mungu atusaidie tuache uvivu. Tuhudumie familia zetu. Bila kujali mke anafanya kazi gani, usihesabu pesa yake, hesabu majukumu yako.

Kama bado hujapata kazi inayoendana na elimu yako nikutie moyo, 2021 Inuka "Kabla hujapata unachotafuta kufanya, fanya kilicho mbele yako" (before you find what you finding to do, do what you find"

Suleman anasema Mhubiri 9 10
"Lo lote mkono wako utakalolipata kulifanya, ulifanye kwa nguvu zako; kwa kuwa hakuna kazi, wala shauri, wala maarifa, wala hekima, huko kuzimu uendako wewe.

Kabla hujafa kama masikini, angalau ionekane umejaribu kuushinda umaskini, maana hakuna aliyeandikiwa umasikini. Wewe ni mzao mteule, umeumbwa kwa mfano wake anaye miliki mbingu na nchi. You're Born A Winner, God can never birth a failure, even once.

Mwanaume ambaye mke wake ndiye anahudumia kila kitu, ni ngumu hata kumuuliza mke wako "unaenda wapi?" maana atakujibu "nisipotoka tutakula nini!, acha nitoke ile tule"

Ukiona ukiulizwa Ada ndiyo unaanza kuwa rohoni, jua kuna shida mahali.

Mwanume kuhudumia familia ni utukufu kwa Mungu, maana ndivyo alivyoumba, mmoja mfanyakazi mmoja msaidizi.

Nimalize kusema, Mithali 13 4
Nafsi ya mtu mvivu hutamani asipate kitu; Bali nafsi ya mwenye bidii itanenepeshwa.

Ukiwa mvivu utatamani amani ya familia, utatamani uheshimiwe, lakini hutopata.

Na kuna wanaume ambao ni wachapakazi, wana pesa ila si wahudumiaji wa wake zao. Ndugu haijarishi kiwango cha pesa ulichonacho. Mwanamke anaheshimu sehemu ya chanzo chake cha heshimu. Mwanamke anapoishi na mwanaume asiyehudumia, hujiona ni bora kuishi na masikini.

Aliyekwambia kumpa zawadi mchumba wako dhambi nani, hata asipokumbuka sms zako, atakumbuka fadhila na utu wako.

Na mwanamke unayesoma ujumbe huu kumbuka...

Mke mwema... "Moyo wa mumewe humwamini, Wala hatakosa kupata mapato" MITH 31:11.

Mwanamke aliyejiweka kuwa mchumba au mke mwema ni, Biblia inasema hatakosa mapato. Hata kama hatofanya, lakini kama wewe ni mke mwema hutokosa mapato. Juhudi yako, ya kuhudumia familia yako, mume akiwa mbali, itaamsha akili yake, na atakuamini na hutokosa mapato.

Nionyeshe mwanamke mchapakazi na ni mwema kwa mumewe, huyo ndiye ambaye Mumewe atamwamini, na hatakosa mapato.

Ubarikiwe Sana.
Kwa Msaada wa Roho Limeandikwa na.
Pastor Ulenje EM.
0683-477827
2021 INAWEZEKANA.


Sunday, January 17, 2021

USIOGOPE, AMINI TU. MARKO 5:36.

 Mathayo 19 26 

 Yesu akawakazia macho, akawaambia, Kwa wanadamu hilo haliwezekani; bali kwa Mungu yote yawezekana.



Mungu anataka tufanikiwe,


Kumbukumbu la Torati 30 15 

 Angalia, nimekuwekea leo mbele yako uzima na mema, na mauti na mabaya;



Mafanikio siyo karama, mafanikio ni uchaguzi. Mungu amekupa kuchagua kufanikiwa au kushindwa. Ila amekupa ushauri, chagua mafanikio.


INAWEZEKANA


1. Ni Kumwambia Mtu, Kuna Njia ya Kufanya ili Hilo Jambo Lifanikiwe.


Inawezekana alijaribu akashindwa kama Musa. Au wenda amejaribu mara nyingi sasa ameona haiwezekani. Au mbele yake anaona giza, hakuna kitu anaona anaweza fanya tena.


Sasa unamwambia INAWEZEKANA.


Katika kila jambo ambalo Mungu anaruhusu litokee kwenye maisha yako, kila mpango una njia ya kufanya. Kuna kitu hujajua tu bado ndiyo maana hujafanikiwa mpaka sasa.


Kuna mambo siyo kwamba hatuwezi ila kuna sehemu, kuna kanuni bado hatuijui.


Katika kila jambo linaloonekana haliwezekani, ni kweli kwamba kuna njia ya kulifanya liwezekane. Hata unayoyaona leo yamefanyika, mwanzo yalionekana hayawezekani.  Mwaka 1904 wana sayansi walikutana Uingereza kuthibitisha kuwa hakuna kitu kinaweza tembea angani. Lakini Ndugu wawili watoto wa Wright maarufu kama Wright Brothers, waligomea maamuzi yale, wakasema inawezekana. Mwaka 1910 wakatembeza ndege kwa mara ya kwanza.


Siyo kwamba haiwezekani, Tatizo umekata tamaa, kutafuta nini unatakiwa ufanye. Bado ipo Njia.


Marko 5:

Mwanamke alitokwa na damu miaka mingi na kuteswa na madaktari wengi, lakini alipogundua njia ya uzima wake. Kuwa nikigusa pindo la Yesu nitapona, akapona. Usikate tamaa, bado kuna kitu unaweza fanya ukafanikiwa.


Si kwamba haiwezekani, ila hujapata mbinu ya Kufanya. Unajua kujua namna ya kufanya mambo kunaondoa miaka mingi ya mateso ba kutoa jasho.


Kumb 2:1-3 Israeli walizunguka miaka mingi ndani ya jangwa wasiione njia. Siku moja Mungu akasema mlivyozunguka mlima huu vyatosha, geukeni upande wa kaskazini.


Israel wakakata tamaa, kuzunguka mda mrefu, siyo kwamba njia ya kufika haikuwepo, ila hawakuijua.


2021 Mungu anakwenda kukupa njia ya kufanya katika Jina la Yesu. Pokea.


Israel walipata neno la Mungu, neno likawaonyesha cha kufanya. Petro alifanya kazi ya kuchosha neno liliposhuka likampa cha kufanya, Mwanamke aliyetokwa na damu miaka 12 alisikia habari za Yesu.


Kuna neno unalihitaji likupe cha kufanya...


A. Soma neno, Yoshua 1:8

B. Omba, Yoshua aliomba. Yoshua 7:6

C. Tafakari, kaa chini fikiri... Mda unaotumia kulia, ungekaa na kufikiri Neno La Mungu linasema nini kuhusu jambo lako na mpango wako, ungekuwa umeshapata njia.

D. Omba ushauri. MITH 13:10.


2. Unamwambia mtu Ambaye Anaona Jambo Au Mpango Hauwezekani.


Wakwanza anaona hakuna njia, huyu wa sasa anaona haliwezekani kabisa. Anaona ni jambo kubwa sana. Anaona ni mpango mkubwa kumzidi. Anaona Ha! Ngoja niwaze mengine, hii ni ndoto tu ya utotoni. Au watu wengi ameona hawajaweza na wengine wamemwambia haiwezekani.


Lakini naomba sikia....


Hakuna jambo haliwezekani kwa mtu aliyeokoka isipokuwa jambo lile ameliona yey mwenyewe kuwa haliwezekani.


Yesu anasema anabisha yupo mlangoni anabisha hodi mtu akifungua nitaingia ndani yake UFUN 3:20.


Aliyeingia ndani yako, Yeye anaweza yote. MATH 19:26 hilo kwa wanadamu haliwezekani ila kwa Mungu yote yanawezekana.


Yoh 14:10 Yesu anasema "bali ni Baba akaaye ndani yangu huzifanya kazi zake"


Kol 1:29 Paulo anasema "nikijitahidi kwa kadiri ya kutenda kazi kwake atendaye kazi ndani yangu kwa nguvu. 


Tangu ulipookoka Mungu anafanya kazi ndani yako.


Fil 2:13 Neno linasema "Ndiye Mungu atendaye kazi ndani yenu, kutaka kwenu na kutenda kwenu, katika kulitimiza kusudi lake jema.


Mungu yupo ndani yako kufanya hilo jambo liwezekane, Mungu aliye ndani yako, kwake yote yanawezekana.


Math 17:20 anasema "

Mathayo 17 20 

 Yesu akawaambia, Kwa sababu ya upungufu wa imani yenu. Kwa maana, amin, nawaambia, Mkiwa na imani kiasi cha punje ya haradali mtauambia mlima huu, Ondoka hapa uende kule; nao utaondoka; wala halitakuwako neno lisilowezekana kwenu.


Maana yake, Ukiona ugumu unaongezeka, badala ya kukata tamaa, wewe amini sana.


Kuona inawezekana ndiyo mwanzo wa kushinda mambo yanayoonekana hayawezekani.


__Yesu alimwambia Yairo (Marko 5:36) "Usiogope, Amini Tu"


Kumbe 2021 Mungu anaposema Yote Yanawezekana, anasema "Usiogope, wewe inua imani yako"


A. Kula chakuka cha imani_ Neno. RUM 10:17

B. Meng'enya hiko chakula_ Tafakari YOSH 1:8

C. Tendea kazi_ Tumia hilo neno. YAK 1:22

D. Usiyumbishwe_ EBR 10:34 usiyumbishwe kile umeamini unapoona ugumu unaongezeka au kwa maneno ya watu.... Yesu hana too late.



3. Unamwambia Mtu Anayeona Hana Uwezo Wa Kufanya.


Anajiona hana uwezo. Hana uwezo wa kifedha, elimu, ndugu, mtaji, upako.


Hakuna mlima mrefu kwa mwanadamu, mlima ni jinsi wewe unavyouona. Maana hata mlima mrefu kuliko yote duniani, watu wameupanda.


Mungu bado hajaumba mwanadamu ambaye hawezi kitu. Alipoumba akasema "ni chema sana" vingine vyote alipotazama akasema ni vema, lakini kwa mwanadamu akasema chema sana.


Mafanikio yana siri hii, Ukijiona huwezi hutoweza. Ila ukijiona unaweza utaweza. Simba siyo mnyama mwenye nguvu kuliko wanyama wote, siyo mnyama mrefu kuliko wanyama wote, wala siyo mnyama menene kuliko wote.... Ila yeye ndiye mfalme wa mwitu.


Kwanini anapokutana nao, wao wanaogopa, ila yeye haogopi yoyote. Hata wale wenye nguvu zana. Tembo anaangusha mti, ila anakutana na simba analiwa, kwanini simba anaona "pamoja ni mnene wewe ni chakula"


Ukiona huwezi hutoweza, kwanini "siku ukisema naweza, basi utatafuta njia kwa kila hari, na utaweza"


Mwanamke mjamzito miezi 8, ilipotokea hatari aliruka ukuta. Aliambiwa rudia alishindwa. Kwanini, mwanzo alipoona hatari, kuna kitu kilisema ndani yake. UNAWEZA.


HESABU 13 MUSA anatuma wapelelezi, Wanarudi wanasema nchi ni nzuri, ila wanajiona hawana uwezo wa kuitamalaki. Wote wanafia jangwani.


Lakini Yoshua na Karebu wakasema "twaweza kushinda bila shaka HES 13:30.


Wengi wanapishana na mafanikio yao, uponyaji wao, majibu ya maombi yao, na kushindwa changamoto sababu wanaona haiwezekani. Inuka sema INAWEZEKANA.


Wanasema "Hakuna cha kufanya" No "Kipo cha Kufanya"


Wanasema "Hakuna Njia" No "Njia ipo" 


Unajua kwanini wanaosema hatuwezi huwa hawawezi "Sababu huwa hawafanyi hiko kitu"


Wanajeshi wa Israel walipoona hawawezi kunshinda Goloathi hata kumfata hawakumfata... Lakini Daudi aliona anaweza, AKAMFATA.... Kwa Jiwe tu Down.


Unachokiogopa na kukiona ni kigumu.... Ni kidogo sana.


Tengeneza ufahamu kuwa Unaweza. Aliye ndani yako ni Mkuu Kuliko Chochote. 


Mungu anatembea na watu wanaosema "Haijalishi Ugumu, Itafanyika"


_________________________



LAKINI KUMBUKA....


Neno linasema "bali kwa Mungu yote yawezekana" 


Maana yake_ Lazima Mungu ahusike. Biblia ya Kingereza inasema "with God, All things are possible"


Mungu hawezi husika mpaka umeomba. Paulo alifanya mambo makubwa ambayo wengine walishindwa, siri yake anasema...


Filipi 4:13 "Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu"


Mungu akikutia nguvu yote yatawezekana kwako.


Maombi, Maombi, Maombi.


Lazima 2021 Tuombe Zaidi ya Miaka Mingine, kama tunataka kufanya yaliyoshindikana yawezekane.


Unapoomba  Unapata Vitu Viwili.


1. Uso wa Mungu_ Unakutana na uso wa Mungu kukupa njia ya kufanya, na nguvu zake.

2. Mkono wake_ wa kukusaidia unapokwama. Israel walikwama Misri na kufanywa watumwa lakini kwa Mkono wake aliwatoa.

3. Roho Mtakatifu_ kusafisha njia na kukufanya iwe unstoppable, uwe na ujasiri, uwe na imani, kukufanya ufanye mambo ambayo wanadamu wa kawaida hawawezi.


Unabii unapotoka unatoka kwa wote, lakini ni maamuzi ya mtu binafsi kufanya unabii utokee kwenye maisha yake. Hauji kuomba kumridhisha mchungaji, ila ni kwa ajili yako, ili upige hatua.


Leo unaona unaenda, ila kuna hatua ili upige ni lazima uombe leo. Kila mtu anakutana na hatua zisizowezekana, na ni hatua zisizowezekana zinawafanya watu wakuzidi kiuchumi na kiroho.


0718 721848

0683 477827

Pastor Ulenje EM