Sunday, January 15, 2023

JITIE NGUVU KATIKA BWANA ILI KUINULIWA NA BWANA

 SOMO LA PILI LA KUINULIWA NA MUNGU


JITIE NGUVU KATIKA BWANA, INUKA


1 SAMWELI 30:1-8

Kujitia nguvu katika Bwana ni kukumbuka ya kwamba yupo Mungu ambaye naweza nikamtegemea, yupo Mungu ambaye nikimtafuta atanipigania na kunipa ushindi.


KWANINI UJITIE NGUVU KATIKA BWANA?


1. KWASABABU BWANA AMETUHIFADHI HAI.

Wakati wa changamoto zote, unachokihitaji hasa ni kuwa hai, kwa sababu ukiwa hai unaweza kugeuza yote uliyokutana nayo kuwa ushuhuda. Kwa sababu majaribu hayawezi kukuharibu kama bado una uhai wa kuendelea kujaribu. 

Pamoja na yote tuliyokutana nayo, ila Bwana alihakikisha yanatuliza, yanatuumiza, yanatuvunja moyo ila hayatuuwi. Siyo kwamba hayakuwa na nguvu ya kutuuwa, ila kwa sababu Bwana alikuwa upande wetu kuhakikisha tunaishi, ili siku moja tuje kusema Farasi na mpanda Farasi aliwatupa baharini. 1 Sam 27:8,9.

Pamoja na yote Daudi aliyokutana nayo, Bwana alihakikisha Suali hamuuwi, alihakikisha Wafilisti hamuuwi, alihakikisha Waamaleki hamuuwi_ kwanini kwa sababu Bwana alitaka kuyageuza yote aliyopitia kuwa kitabu cha SIFA CHENYE SURA nyingi kuliko zote kwenye Biblia 150. 

Biblia inasema Mhubiri 9:4 Kwa kuwa liko tumaini kwa yule aliyeambatana na wote walio hai; (maana ni afadhali mbwa aliye hai kuliko simba aliyekufa);

Maadamu Una Uhai, Bado Lipo Tumaini, Inuka Jitie Nguvu Katika Bwana.


2. KWA SABABU MACHOZI TULIYOLIA HAYAJATUTOA TULIPO TEKWA.

Daudi na wenzie mianne wakainua sauti zao na kulia, siyo tu walilia, bali waliinua sauti zao na kulia mpaka walipokuwa hawana nguvu za kulia tena; lakini majibu hayakutokea. Wakaanza kumlaumu Daudi lakini lawama hazikuwasaidia.

Mungu ameweka machozi ili kutujulisha kwamba kuna jambo la uchungu, ila siyo njia ya kututoa kwenye uchungu. Mungu ameweka machozi ili watu wajue kuwa upo matekani, ila siyo ya kukutoa kwenye mateka. Kama umeamua kulia ni bora ulie kuinuka kwa mkono wa Bwana ili siyo ulie kuonyesha namna unapitia. Adui amekuteka ili ulie, unapolia unampa sifa kuona amekuweza. Daudi akainuka, akajitia nguvu katika Bwana, ndipo ukombozi wao ukapatikana. 


Kama machozi hayajakupa matokeo, Leo inuka Jitie Nguvu katika Bwana, Mungu wako Anakusubiri umalize kulia na kulalamika ili Akusaidie. 

Wakati Daudi na wenzie wanalia, Mungu alikuwa akiwatazama, ila Daudi alipojitia nguvu, Mungu akainua mkono wake na kuwainua na hapo ukawa mwanzo wa Daudi kuwa Mfalme na wenzie kuwa majemedari wa jeshi na wakuu wa Israel ambao hapo kwanza walimfata Daudi sababu walikuwa na njaa na madeni.


3. KWA SABABU BWANA AMEHAKIKISHA TUNABAKIWA NA NAIVERA.

Wakati adui anateka vyote kuhani tulibakiwa naye, na naivera nayo ikabaki. Naivera lilikuwa ni vazi la kikuhani, ambalo kuhani alivaa anapojihudhurisha kwa Bwana, na ni vazi lilibeba majina ya makabila ya wana wa Israel. 

Adui ameiba vyote, ila damu ya Yesu bado tunayo, ambayo haishindwi kwa dhambi zetu, haishindwi kwa nguvu za adui, haishindwi kwa nguvu ya pesa, adui ataiba vyote ili naivera bado tunayo, vazi la damu ya Yesu bado tunalo ambalo kwa hilo tunasogea mbele za Mungu wetu na kupokea nguvu mpya ya kumshinda adui aliyetushinda.

Ebrania 4:16 Basi na tukikaribie kiti cha neema kwa ujasiri, ili tupewe rehema, na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji.

Maadamu bado una vazi la damu ya Yesu, Acha kubaki chini, Jitie nguvu katika BWANA 2023, inuka.


4. JITIE NGUVU KATIKA BWANA KWA SABABU UKIFUATA UTAYAPATA. 

Daudi alipoacha kulia na kujitia nguvu katika Bwana, ndipo Bwana anamwambia, Inuka_ Ukiwafuata utawapata na utawapokonya yote waliyoiba, yote waliyochukua. Kumbe tunayofikiri hayawezi kuisha, yanaweza kuisha, yale tunasema hatuwezi kupita, tunaweza kupita, yale tunawaza hayawezi kutuachia, yanaweza kutuachia; 

Lakini kama tutainua imani, na kujitia nguvu katika Bwana, basi tutavipata. Kwa nini, kwa sababu Bwana ameshaondoa nguvu zilizo juu yao.

Yoshua na Kalebu wakawaambia makutano; Lakini msimwasi BWANA, wala msiwaogope wale wenyeji wa nchi, maana wao ni chakula kwetu; uvuli uliokuwa juu yao umeondolewa, naye BWANA yu pamoja nasi; msiwaogope. Hesabu 14:9.

Unayoyaogopa yameondolewa nguvu zake, unayosema yanakutesa, yanakuliza, ni magumu, huwezi kutoka; yameondolewa nguvu zake_ tatizo siyo yenyewe tena, tatizo ni wewe hutaki kuinuka na kuyafuatia. Ukiyafuatia utayapata_ Ukiinuka na kupigana utashinda.

Kumbe tunavyohofu hatuwezi kuvipata, hatuvipati kwa sababu tunahofu ya kutokuvipata, kumbe kesho tunayohofu itakuwa mbaya, siyo kwamba ilitakiwa kuwa mbaya, inakuwa mbaya ni kwa sababu hatujaifuta tumeacha siku zote itufate sisi, YESU anasema 

Basi msisumbukie ya kesho; kwa kuwa kesho itajisumbukia yenyewe. Yatosha kwa siku maovu yake. Math 6:34.

Kesho imewekwa ijisumbukie yenyewe, wewe ifuate kwa imani, maovu ya leo yasikukatishe tamaa maana siku inatosha kwa maovu yake.

Bado Lipo Tumaini, Kama utajitia nguvu katika Bwana, Utawapata Hakika


Mimi ni Pastor Ulenje 

+255 683 477827 

pastorulenje@outlook.com 

Nifatirie kupitia mitandao ya Kijamii 

Tiktok, Facebook, Youtube na Instagram kwa Jina la Pastor Ulenje.



No comments:

Post a Comment