Wednesday, January 25, 2023

SOMO MAALUMU LA KUINULIWA NA MUNGU #04

 SOMO LA NNE

KUMKUMBUKA HULINDA AGANO LA KUINULIWA


Bali utamkumbuka BWANA, Mungu wako, maana ndiye akupaye nguvu za kupata utajiri; ili alifanye imara agano lake alilowapa baba zako, kama hivi leo. Kumb 8:18 

Ndiyo! Utainuliwa lakini unahitaji zaidi ya kuinuliwa unahitaji kubaki katika kuinuliwa. Maana mara nyingi tumeshuhudia kwenye maisha yetu up and down sasa ukiendelea kupanda na kushuka hautafika popote. Bali ili ufike mbali ni lazima ukiwasha ndege yako kupaa ni moja kwa moja.

Neno la leo ni neno la kulihifadhi, sababu Mungu anaanza kukuinua kidogo kidogo sasa, hili neno litakusaidia kubaki kwenye sehemu ya kuinuliwa, kuzidishwa na kuongezwa daima.

KUMB 8:1_ Musa anawaambia Amri hii ninayokuamuru leo mtaishika kuitenda, mpate kuishi na kuongezeka, na kuingia katika nchi ile ambayo BWANA aliwaapia baba zenu; nanyi mtaimiliki.

KANUNI #04 MUHIMU ILI KUBAKI KUINULIWA BILA KUSHUKA CHINI

#01. KUMBUKA MUNGU ALIPOKUTOA NA NAMNA ALIVYOKUINUA.

Mungu aliwapa amri  ya kumkumbuka ili wabaki kwenye kuongezwa, sababu alijua mwanadamu huwa anakumbuka akiwa hana, ila akipata anasahau; anasahau alipotoka, anasahau namna alivyofika alipo, na hasa anasahau aliyemuinua, hata akijitazama anaona ni kwa uwezo wake na ubora wake amefika pale.

KUMB 8:2, 12-14 ___Musa anawaambia Nawe utaikumbuka njia ile yote BWANA, Mungu wako aliyokuongoza miaka hii arobaini katika jangwa,

12 Angalia, utakapokuwa umekula na kushiba, na kujenga nyumba nzuri na kukaa ndani yake;

13 na makundi yako ya ng’ombe na kondoo yatakapoongezeka, na fedha yako na dhahabu yako itakapoongezeka, na kila kitu ulicho nacho kitakapoongezeka;

14 basi hapo moyo wako usiinuke, ukamsahau BWANA, Mungu wako, aliyekutoa katika nchi ya Misri, katika nyumba ya utumwa;

Watu wengi wasipokuwa na kazi wanamtafuta Mungu, wakiwa hawana biashara, hawana mume, lakini wakipata basi wanatumia kazi, mume, biashara kama kisingizio kuwa hawawezi tena kuja kanisani kumtafuta Mungu. Wanasahau kuwa Mungu aliyewapa alijua kuwa huwezi firisika kama utampa muda. 

Hakuna mtu anaweza firisika kwa kumpa Mungu muda.


#02. MUNGU ANATUPELEKA JANGWANI KUTUFUNDISHA UNYENYEKEVU.

Shika hili Mungu anatuongozwa njia ya jangwani ili kutupeleka kwenye mafanikio, ili tujue kuwa Yeye ndiye mpaji wetu. Kuna watu jangwani wanafikiri ni wakati ambao hauna kitu cha kula wala kuvaa, hapana huyo siyo Mungu ni shetani kemea kwa Jina la YESU.

Mungu anatupeleka jangwani ili atuonyeshe kuwa yeye ni mpaji ___yaani anatuongoza sehemu ambayo tunakuwa hatuna uwezo wa kupata chakula wala mavazi kwa uwezo wetu alafu yeye anatupatia vyote hivyo na kuzidi bila hata juhudi zetu. Anafanya hivyo ili tujue kuwa yeye ndiye mpaji wetu.

KUMB 8:2, 3 Musa anawaambia Israel__

2 Nawe utaikumbuka njia ile yote BWANA, Mungu wako aliyokuongoza miaka hii arobaini katika jangwa, ili akutweze, kukujaribu kuyajua yaliyo moyoni mwako, kwamba utashika amri zake, au sivyo.

3 Akakutweza, akakuacha uone njaa, akakulisha kwa mana, usiyoijua wewe wala baba zako hawakuijua; apate kukujulisha ya kuwa mwanadamu haishi kwa mkate tu, bali huishi kwa kila litokalo katika kinywa cha BWANA.

Israel walichukua miaka 40 kujifunza kuwa Mungu ni mpaji sababu walitaka sana kutumia nguvu zao. 

Kama utajifunza mwaka huu kuwa Mungu wako ndiye mpaji, na ya kuwa utakumbuka amri zake na kumkumbuka wakati wa kuongezeka, utakumbuka kuwa wakati upo jangwani ndiye alikulisha na halo ulipofika si kwa uwezo wako, basi atakuinua, Musa anasema alikujaribu ayajue ya moyoni mwako,

Kumbe kuna wakati Mungu anatupeleka sehemu ambapo tutakosa vitu, lakini atafanya tule tuvae ili ajue mioyo yetu kama itasema asante na kumtazama yeye peke yake bila kulalamika bali kuamini kuwa Yeye ndiye mpaji wetu. 


#03. TUNATAKIWA KUMKUMBUKA MUNGU SABABU YEYE NDIYE ATUPAYE NGUVU YA KUPATA UTAJIRI.

Nguvu ya kupata utajiri ni pamoja na ufahamu, nguvu, baraka, neema, kibali, na afya. Vyote hivi ni Mungu ndiye atupaye. Maana yake unatakiwa kumkumbuka sababu yeye ndiye atoaye hizo nguvu za kupata utajiri. 

KUMB 8:13, 14 __Musa anasema;

13 na makundi yako ya ng’ombe na kondoo yatakapoongezeka, na fedha yako na dhahabu yako itakapoongezeka, na kila kitu ulicho nacho kitakapoongezeka;

14 basi hapo moyo wako usiinuke, ukamsahau BWANA, Mungu wako, aliyekutoa katika nchi ya Misri, katika nyumba ya utumwa;

Musa anaongea kuhusu kutuongeza, kumbe kuna wakati Mungu ataanza kutuongeza. Neno linasema usimsahau BWANA Mungu wako. Kwanini, kwa sababu maongezeko huwa yanasababisha ulevi wa vitu, majigambo, na ubize __ mali ikiongezeka ina tabia ya kuchukua nafasi ya Mungu.

Kwanza lazima ujue Mungu hayupo kinyume na wewe kuwa tajiri ndiyo maana anatoa nguvu ya kupata utajiri, ila hataki mali ichukue sehemu yake; ndiyo maana anayemkumbuka wakati wa kuongezwa huwa anamuongeza zaidi.

Mungu sasa anakuongeza ndiyo maana ulichonacho leo hukuwa navyo jana, sasa kama utamkumbuka Mungu kwa maongezeko madogo basi atakuongeza sana na sana. 


#04. KUMKUMBUKA KUNAFANYA IMARA AGANO LA KUINULIWA.

KUMB 8:18 Musa Anaweka wazi __Bali utamkumbuka BWANA, Mungu wako, maana ndiye akupaye nguvu za kupata utajiri; ili alifanye imara agano lake alilowapa baba zako, kama hivi leo.

Anasema ili alifanye imara agano lake. Kumbe kumkumbuka ndiko kunaleta kufanywa imara agano la kuongezeka. 

Kuongezwa ndiko kunaleta kuinuka. Ana maanisha anakuongeza sawa, lakini usiridhike, mkumbuke hapo atafanya imara zaidi hilo agano lake la kukuongeza. Maana yake ndipo utaendelea kuongezeka na kuongezeka.

Galatia 3:9 __ Basi hao walio wa imani hubarikiwa pamoja na Ibrahimu aliyekuwa mwenye imani.

Baraka ya Ibrahimu ni kuongezwa na kuzidishwa, lakini utaona Ibrahimu alishika agano, na kwa kushika kwake agano aliinuka siku zote bila kushuka chini.

2 Kor 9:8 Na Mungu aweza kuwajaza kila neema kwa wingi, ili ninyi, mkiwa na riziki za kila namna siku zote, mpate kuzidi sana katika kila tendo jema;

Kumbe Mungu huwa anatujaza neema ili tukiwa na riziki tuzidi kuteda mema. Maana yake Mungu anakuongeza kidogo kwanza ili apime moyo wako, bidii yako ya kumkumbuka na kumuweka mbele inakupa kukuongeza siku hata siku.


Ubarikiwe Sana, Fanyia kazi haya uliyosoma hakika utaona Kubarikiwa Sana. 

MAOMBI

Eh! Mungu Baba nisaidie siku zote hata wakati nikiongezeka nisikusahau wewe, uniweke sehemu ya kuinuliwa na wewe siku zote. 

Mimi ni Pastor Ulenje 

+255 683 477 827, pastorulenje@outlook.com 



No comments:

Post a Comment